Simba ni mnyama ambae amekuwa akijulikana kama mfalme wa mwitu au King of the Jungle, na kila mnyama mwingine akimwona simba huyu, anaogopa na kukimbia.
Nimekua nikijiuliza kwa nini simba amekua mnyama wa kuogopwa sana, na amechukuliwa kama kiongozi wa wanyama wote katika ulimwengu wa wanyama?
Simba huyu sio mrefu kuliko wanyama wote, kama urefu ungekua kigezo angekua Twiga!
Simba sio mkubwa kuliko wanyama wote, kama urefu ungekua kigezo angekua Tembo!
Hana nguvu nyingi kama kiboko au nyangumi hata kupindua meli kubwa kama nguvu ingekua kigezo!
Simba huyu si mkali kuliko wanyama wote!
Wala si mnyama mwenye sumu kali kuliko wanyama wote!
Sasa kwa nini yeye ni kiongozi wa wanyama wengine wote unapozungumzia wanyama?
Ametumika sehemu mbalimbali kama ishara ya nguvu, ushindi, na utawala!
Nilipata interest ya kujifunza juu ya mnyama huyu ili kujua siri yake ni nini?
Mungu huwa anatumia mambo ya kawaida yanayomzunguka mwanadamu ili kumfundisha mambo makubwa na kumhekimisha!
Simba anapokutana na wanyama wengine ana kwa ana, unafikiri nani huwa anaogopa na kumkimbia mwenzake? Ni wanyama wengine au Simba?Kwa nini?
Bila shaka ni wale wanyama wengine, na hata kama ni kundi la wanyama wengi, bado wanapomwona simba huwa wanakimbia kuyanusuru maisha yao!
Unafikiri ni kwa nini?Kwa nini asingekua simba ndiye alitakiwa kukimbia kwa sababu wale wanyama huenda ni wengi?
Nilijifunza kitu kutoka kwa Simba.
Na kitu hicho ni MTAZAMO au ATTITUDE!
Simba anapomwona mnyama yeyote yeye huwa anaona MSOSI! Anaona na kuwaza huu ni msosi kwangu, au ni chakula kwangu cha siku ya leo. Lakini yule mnyama mwingine akimwona simba, yeye anaona KIFO!
Wanyama hawa wawili wana mitazamo tofauti mmoja anapokutana na mwingine, na mitazamo hiyo ndio inapelekea kila mmoja kufanya kitendo ambacho atakifanya. Mmoja atakimbia kujihami na kifo, na mwingine (Simba) atakimbilia mawindo yake, apate kitoweo.
Wewe unapokutana na jambo, mtazamo kuhusu hili jambo huwa ni nini? Mtazamo wako juu ya hilo jambo ndio utakaopelekea wewe kuchukua maamuzi utakayo chukua ambayo yatakuletea matokeo yatakayoonekana kwa nje.
Kwa mfano unapopokea taarifa kuhusu jambo fulani, nini kinakufanaya ufurahi au ukasirike? Ni mtazamo wako juu ya hilo jambo.
Mtakua wawili, mtapewa taarifa moja, lakini mmoja atalia na mwingine atacheka, kwa nini? Ni mtazamo alionao mmoja juu ya lile jambo umetofautiana na mtazamo alionao mwingine juu ya jambo hilo hilo.
Kuna fursa nyingi sana watu hukosa kwa sababu ya mtazamo walionao juu ya watu wa jambo Fulani.
Utakapoamua kubadilisha mtazamo wako juu ya hali Fulani unayopitia utashangaa namna ambavyo utaanza kuona suluhisho la hilo jambo.
..ungana nami wiki ijayo siku kama ya leo tuendelee na mfululizo huu..
~Mwl Minna