Tunapokea taarifa kutoka wa watu mbalimbali kila siku na taarifa kutoka sehemu mbalimbali,lakini inategemea sana tunapokeaje taarifa tulizopewa na tunaamini taarifa ipi kati ya tulizopokea!
Matokeo ya maamuzi yetu yatatarajia jinsi tulivyo pokea taarifa tulizopewa na kuzipambanua ili kujua tufikie maamuzi gani.
Mara zote maisha yetu ni matokeo ya maamuzi ambayo tumeyafanya baada ya kupokea taarifa fulani wakati fulani katika maisha.
Wengine wamekuwa kwenye fani fulani kwa sababu tu walipokea taarifa kuwa hiyo fani miaka ijayo itakua na soko kwa hiyo wakaisomea hiyo.
Mwingine yuko kwenye ofisi aliyoko kwa sababu, alipata taarifa kuna tangazo la kazi au kuna uhaba wa wafanyakazi hivyo aombe kazi hapo, na akapata.
Mwingine akianzisha biashara fulani kwa sababu alisikia kwamba inafaida na ndio akaamua kutupia mtaji wake hapo, na kadhalika na kadhalika.
Kwa hiyo maisha ni mjumuiko wa maamuzi tunayofanya kila siku, na maamuzi hayo yanatokana na taarifa tunazopokea.
Unapoenda hospitali, mathalani unakua unaumwa au umeenda kufanya 'check up' ya mwili, unatarajia taarifa ya daktari, na ikija unaamini hivyo ndio hali ya mwili wako ilivyo,lakini kuna wakati majibu yanatoka kwa daktari na hayakuridhishi, hivyo unachukua hatua ya kwenda sehemu nyingine ili kuhakikisha kwamba yale majibu ya daktari ni sahihi au hayakua sahihi.
Mwanafunzi anapofanya mtihani anasubiri matokeo kutoka kwa mwalimu wake,na majibu yatakapotoka, ndio taarifa ya matokeo yake,na matunda ya kisomo chake kw a muda wote aliokua anasoma.
Lakini pia kama mwanafunzi huyo atakua hajaridhika na matokeo ya mtihani wake kutoka kwa mwalimu wake, anahaki na kuhoji matokeo yake,na anapewa ruhusa na kukata rufaa,ili mtihani wake uangaliwe kwa mara nyingine, ili kama ulisahihishwa kwa makosa urekebishwe nae apewe matokeo yake sahihi.
Taarifa nyingi hutujia kila siku, nyingine hufurahisha na nyingine huwa si nzuri wenye masikio yetu.
Kuna wakati simu ikipigwa moyo unashtuka kwa sababu unadhani inaweza ikawa si taarifa nzuri sana kuisikia. Na wakati mwingine tuna kimbilia kuuliza kama taarifa unazotarajia kusikia ni njema,ili kuuandaa moyo kukabiliana na taarifa unazoenda kupokea.
Lakini kuna wakati mwingine unapoona tu namba ya simu, huachi ikalia mara ya pili, umeshapokea kwa sababu unajua kuna hiyo simu imebeba taarifa nzuri ambazo huwezi kusubiri kuzisikia.
Taarifa unazozipata kila siku zinatokana na watu wanaokuzunguka iwe majirani, wafanyakazi wenzio,marafiki, mtandaoni,au kokote ambako kuko karibu na wewe.
Hivyo basi swala la nani anakuzunguka ni muhimu kuliangalia kwa umakini ili kupata taarifa sahihi na muhimu zitakazo wezesha wewe kufanya maamuzi sahihi katika kile unachotaka kutimiza.
Wakati wana wa Israel wana endelea na safari chini ya uongozi wa Mussa (Hesabu 13),walitakiwa kwenda kufanya uchunguzi wa mji wa Kanaan ambao Mungu alikua akiwaongoza kwenda kumiliki. Nawalienda kundi la watu kumi na mbili, miongoni mwao wakiwemo Joshua na Kalebu.
Watu hawa walifika katika mji ule,na kuukuta na wote waliona walioyakuta, lakini kila mmoja alipokea taarifa ile tofauti na kuipeleka kwa Mussa na wana wa Israel kama walivyoipokea.
taarifa yao ilitegemewa sana ili kuwawezesha wana wa Israel kuendelea na safari wakiwa na nguvu na ari ya kuufikia mji ambao Mungu aliwaahidi tangu wakiwa utumwani Misri.
Waliipeleleza ile nchi na kukuta ni nzuri na imejaa maziwa na asali. Lakini watu wanaokaa katika nchi ile ni hodari, na miji yao ina maboma, nayo ni makubwa sana; na pamoja na hayo waliwaona wana wa Anaki( kabila la watu waliokuwa na nguvu na warefu sana(giants))
Wakarudi na kupeleka taarifa, taarifa ambayo ilikua inategemewa sana na waIsrael.
Pamoja na taarifa nzuri ambayo Joshua na Kalebu walitoa, wale walioenda pamoja nao, wakaleta taarifa mbaya sana kuhusu ile nchi, kwamba "ile ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno.Tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi."
Ukiendelea kusoma Hesabu 14 utaona kwamba kutokana na ile taarifa mbaya waliyoipata,walinung'unika mbele za Mungu na kulalamika na kumkasirisha Mungu, matokeo yake hawakuingia katika ile nchi ya ahadi. Kundi loote lililotoka Misri,isipokua Joshua na Kalebu, hawakuiona kaanan, wote walifia jangwani.
Mpendwa msomaji wangu, unaweza kuona jinsi gani taarifa tunazopokea zinavyoweza kusababisha kufa kwa lile kusudi ambao tunakazana kulitimiza. Watu hawa walibakisha sehemu ndogo sana ili kufika mwisho wa safari, lakini wakafia njiani.
Mara ngapi tumekua na maono na ndoto za kufanya vitu vikubwa lakini katikati ya safari tunapokea taarifa hasi(negative information) ambazo zinasababisha tushindwe kuendelea katika safari ya kutimiza ndoto zetu?
Ni jambo la muhimu sana kuhakikisha taarifa tunazopata hazizuii sisi kuendelea na safari yetu.Ni kweli kwamba kwenye nchi waliyoenda kupeleleza kulikua na majitu, lakini haikutakiwa kuwa kikwazo kwa wana wa Israel,kwa sababu tayari walisha hakikishiwa na Mungu wao ushindi!kwa sababu aliye ndani yao ni mkuu kuliko aliye katika ulimwegu.
Kama Daudi angemwogopa Goliath kwa sababu ya taarifa ambazo alisikia kuhusu yeye asingeweza hata kumsogelea.Lakini alichagua kutokusikiliza zile taarifa za kukatisha tamaa na aliamua kusikiliza taarifa ambazo Mungu alimwambia, kuwa yeye yuko pamoja nae, kwamba yeye ni mwamba wa wokovu wake, kwamba, yeye ni Mungu wa wote wenye mwili na hakuna jambo gumu asiloweza..
Mpendwa msomaji,ni muhimu kuwa makini na taarifa unazopokea kila siku kwani ndizo zinazotegemea maamuzi unayoyafanya kila siku, na matokeo ya maisha yako ni jumla ya maamuzi unayoyafanya kila siku.
Mungu akubariki!
firmina.matee@gmail.com
No comments:
Post a Comment